Kaimu Kamanda Kikosi Mgulani JKT Meja Heri Mwakalebe amewahasa wanafunzi wa kidato cha kwanza na waliohamia shule hiyo kuepusha na makundi yasiyofaa ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao.
Meja Mwakalebe ameyasema hayo leo tarehe 4 Machi 2022, akiwa Mgeni Rasmi katika ufungaji wa mafunzo ya ukakamavu na uzalendo kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza na wanafunzi waliohamia katika Shule ya Sekondari ya Jitegemee jijini Dar es Salaam.
"Wanafunzi acheni kujihusisha na makundi yasiofaa ili kujiepusha kuingia katika vishawishi vya matumizi mabaya ya dawa za kulevya na tabia nyingine zisizofaa" alisema Meja Mwakalebe.
Meja Mwakalebe amewataka wanafunzi hao kutumia muda wao kusoma ili kutimiza ndoto za maisha yao kwa kupata elimu bora ili kupambana na adui ujinga ambaye ni chanzo cha maradhi na umaskini.
Vilevile, amewahimiza wanafunzi wa kike kujiepusha na vishawishi mbalimbali badala yake wajifunze kutoka kwa wanawake waliofanikiwa na kufanya vizuri kwa kuwa viongozi katika Taifa.
Aidha, Meja Mwakalebe ametoa rai kwa shule nyingine ambazo hazitoi mafunzo hayo kuiga mfano wa shule ya Sekondari ya Jitegemee ya kutoa mafunzo ya ukakamavu kwani yanawafanya wanafunzi kuwa wakakamavu na wazalendo kwa nchi yao.
Nae Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari jitegemee Meja Mao Warioba ameeleza kuwa wanafunzi waliopata mafunzo hayo ambao wamejiunga na kidato cha kwanza ni 125 na 12 ni wa vidato mbalimbali ambao wamehamia shuleni hapo .
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wanafunzi hao wa kujitegemea, kujiamini, kuwa na nidhamu, kuwa wavumilivu na wazalendo.
Pia, amewasisitiza wazazi wa wanafunzi hao kuwa wa kwanza kutoa mafunzo mbalimbali kwa watoto wao ili kuwajenga katika misingi mizuri kuanzia ngazi ya familia.
Awali, Meja Warioba ameeleza kuwa Shule ya Sekondari jitegemee ni zao la sera ya utoaji Elimu ya Sekondari kwa watu wazima ambapo mwaka 1974 kilianzishwa kituo cha Elimu ya watu wazima kwa ajili ya kuwapatia Askari na Maafisa ambao hawakuwa na elimu hiyo, kituo hicho kiliitwa Mgulani JKT Sekondari.
Comments
Post a Comment