Waziri wa Ulinzi na JKT Mhe. Innocent Bashungwa amelipongeza Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), kwa kuendelea kutekeleza jukumu la malezi ya Vijana kupitia mafunzo yao ya Kujitolea na Mujibu wa Sheria yanayotolewa kwenye makambi ya JKT ili kuwajengea uzalendo pamoja na stadi za kazi na waweze kushiriki ujenzi wa Taifa.
Mhe. Bashungwa amesema hayo alipofanya ziara ya kikazi iliyolenga kujitambulisha, Makao Mkuu ya JKT Chamwino, Jijini Dodoma ambapo alipata fursa ya kuongea na Maafisa, Askari, Vijana na Watumishi wa Umma wanaofanyia kazi JKT eneo la Dodoma.
Mhe. Bashungwa ameongeza kuwa, Kukamilika kwa miradi ya Kilimo cha kimkakati katika shamba la SUMAJKT lililopo Mngeta na Ujenzi wa miundombinu ya Skimu ya Umwagiliaji iliyopo katika kikosi cha Chita JKT
mkoani Morogoro, Italeta tija katika upatikanaji wa chakula cha kutosha na kulihakikishia Taifa Usalama wa Chakula pamoja na upatikanaji wa Mbegu bora. Ameongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita imetenga bajeti ya fedha kupitia Wizara ya Ulinzi na JKT kwenye Sekta ya kilimo kwa ajili ya ununuzi wa mitambo na zana za kilimo ili kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali yakiwemo ya kimkakati kupitia vikosi vya JKT.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Innocent Bashungwa akifuatilia Taarifa za Shughuli zinazofanywa na Jeshi la Kujenga Taifa Katika Ukumbi wa Mkutano Makao Makuu ya JKT yaliyopo Chamwino Jijini Dodoma.
Mhe. Bashungwa ameeleza kuwa ili Vijana wanaomaliza Mafunzo ya JKT wakalete mabadiliko chanya kiuchumi, ni muhimu kwa JKT, Wizara na Wadau wengine kushirikiana ili kundi hilo kubwa la Vijana wanaomaliza mkataba wa kujitolea wapate ushawishi wa kujiajiri kupitia shughuli za Uzalishaji Mali ikiwemo Kilimo.
Aidha, Mheshimiwa Bashungwa ameushukuru Uongozi wa JKT chini ya Meja Jenerali Rajabu Mabele kwa maandalizi makubwa ya mapokezi yaliofanyika ambapo amehaidi kushirikiana na JKT katika kutekeleza majukumu mbalimbali chini ya Wizara ya Ulinzi na JKT anayoingoza.
‘’Nakushukuru sana Mkuu wa JKT na timu yako kwa mapokezi mazuri na Taarifa ya Utendaji wa majukumu ya JKT, Mikakati na Changamoto ambayo imenipa picha kamili na uelewa mkubwa wa Utendaji kazi wa JKT’’. Alisema
Naye Mkuu wa JKT Meja Jenerali Rajabu Mabele amempongeza Waziri Bashungwa kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi na JKT na kuahidi kuwa JKT litampa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu yake ndani ya JKT.
Kwa upande wake Mkuu wa Tawi la Utawala JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema kuwa JKT linatekeleza majukumu yake katika vikosi na makambi yake pamoja na Chuo cha Uongozi cha JKT kilichopo Kimbiji Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Innocent Bashungwa akipokea Katika hatua nyingine, Zawadi kutoka kwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa Meja Jenerali Rajabu Mabele.
Waziri wa Ulinzi na JKT Mhe. Innocent Bashungwa katika ziara hiyo aliyoifanya Makao Makuu ya JKT ameambatana na baadhi ya Wawakilishi wa Wakuu wa Matawi kutoka Makao Makuu ya JWTZ na Wizara ya Ulinzi na JKT pamoja na Wasaidizi kutoka katika ofisi yake.
Comments
Post a Comment